Episode Details
Back to Episodes
Kumbuka Mikono Iliyokushika Ulipokuwa Unaanguka!
Description
🎙️ Leo kwenye Neno la Leo
Leo kupitia 2 Samweli 19:31–39 tunakutana tena na Barzilai, mmoja wa watu waliomsaidia Mfalme Daudi alipokuwa amekimbia Yerusalemu kutokana na uasi wa mwanawe Absalomu.
Unamkumbuka Barzilai?
Huyu ndiye aliyekuwa miongoni mwa watu waliomletea Daudi chakula na mahitaji mengine alipofika Mahanaimu akiwa amechoka na bila uhakika wa kesho yake.
Lakini sasa mambo yamebadilika.
Daudi aliyekuwa akikimbia sasa anarudi kwenye ufalme wake.
Na katika safari yake ya kurudi, hamusahau Barzilai.
Anamwalika aende naye Yerusalemu ili aweze kumtunza kama ishara ya shukrani kwa wema aliomtendea.
Lakini Barzilai, akiwa na umri wa miaka 80, anaomba arudi nyumbani kwake na anapendekeza Kimhamu aende badala yake.
Daudi anakubali na kumuaga kwa heshima.
Na hapa tunajifunza jambo muhimu sana:
Usiwasahau watu waliokusaidia wakati hukuwa na kitu cha kuwarudishia.
Katika maisha yetu, kuna watu ambao wamekuwa sehemu muhimu ya safari zetu.
Wapo waliotupa nafasi ya kwanza wakati hakuna aliyetuamini.
Wapo waliotusaidia wakati tulipokuwa na mahitaji.
Wapo waliotusikiliza, kututia moyo na kusimama nasi wakati mambo yalipokuwa magumu.
Lakini tunapopata mafanikio, je, bado tunawakumbuka?
Katika 1 Wathesalonike 5:18 tunakumbushwa kushukuru katika kila hali. Na Waebrania 6:10 inatukumbusha kwamba Mungu hasahau kazi ya upendo.
Daudi hakumsahau Barzilai baada ya kutoka katika shida.
Na leo tunakumbushwa kwamba shukrani haipaswi kuishia kwenye maneno tuliyosema wakati tulipokuwa tunahitaji msaada.
Inaweza kuonekana pia katika namna tunavyowathamini watu baada ya hali zetu kubadilika.
Kwa hiyo leo jiulize:
Ni nani aliyekuwa Barzilai katika maisha yangu?
Ni nani aliyenisaidia wakati nilikuwa sina uwezo, nafasi au matumaini?
Na swali muhimu zaidi:
Je, nimewahi kuchukua muda kumshukuru?
Huenda leo ni siku nzuri ya kumpigia simu, kumtumia ujumbe au kumwonyesha kwamba bado unakumbuka wema wake.
Kwa sababu mafanikio yako hayapaswi kukufanya usahau watu waliokuwa sehemu ya safari yako.
Karibu tusikilize, tutafakari na kujifunza pamoja. 🙏📖✨