Episode Details

Back to Episodes
Hata Baada ya Kupoteza, Bado Unaweza Kuanza Upya!

Hata Baada ya Kupoteza, Bado Unaweza Kuanza Upya!

Season 4 Episode 26 Published 2 days, 7 hours ago
Description

🎙️ Leo kwenye Neno la Leo

Leo kupitia 2 Samweli 19:14–15 tunafika katika hatua mpya ya safari ya Mfalme Daudi.

Baada ya kukimbia Yerusalemu kutokana na uasi wa mwanawe Absalomu, kupitia vita na hatimaye kumpoteza mwanawe, sasa Daudi anapata nafasi ya kurudi nyumbani.

Watu wa Yuda wanakubaliana kumkaribisha tena kama mfalme wao.

Na Biblia inasema:

“Basi mfalme akarudi, akafika Yordani.”

Maneno haya yanaonekana rahisi lakini yana ujumbe mkubwa.

Daudi aliyekuwa amekimbia sasa anarudi.

Lakini hebu fikiria jambo moja.

Daudi harudi akiwa na kila kitu alichokuwa nacho kabla ya kuondoka.

Absalomu hayupo tena. Maumivu ya familia yake hayajafutika na mambo mengi hayatakuwa kama zamani.

Lakini licha ya yote aliyopitia, safari yake haijaishia jangwani.

Na hapa tunajifunza jambo muhimu sana kuhusu maisha.

Wakati mwingine tunapitia misimu ya kupoteza, kuvunjika moyo, kushindwa au kuanza upya.

Tunatamani mambo yarudi kama yalivyokuwa zamani. Tunatamani turudishiwe kila tulichopoteza.

Lakini wakati mwingine kuendelea mbele hakumaanishi kurudishiwa kila kitu.

Kunamaanisha kupata nguvu na neema ya kuendelea hata ukiwa umebeba kumbukumbu za yale uliyopitia.

Katika 2 Wakorintho 4:8–9, Paulo anatukumbusha kwamba tunaweza kuangushwa lakini tusiangamizwe.

Na Zaburi 30:5 inatukumbusha kwamba kilio kinaweza kukaa usiku lakini asubuhi ikaja furaha.

Kwa hiyo leo jiulize:

Je, kuna sehemu ya maisha yangu ambayo nimeamini kwamba kwa sababu nilivunjika, basi safari yangu imekwisha?

Huenda mambo hayatakuwa kama zamani. Huenda kuna vitu ambavyo haviwezi kurudi.

Lakini hilo halimaanishi kwamba hakuna tena maisha, matumaini au hatua mpya mbele yako.

Usijilazimishe kuwa mtu yuleyule uliyekuwa kabla ya maumivu. Lakini pia usikubali maumivu yawe mwisho wa hadithi yako.

Daudi aliondoka Yerusalemu akiwa katika maumivu na hofu. Sasa anaanza safari ya kurudi.

Na leo tunakumbushwa kwamba:

Kurudi nyumbani si lazima kumaanishe kila kitu kimerudi kama zamani. Wakati mwingine kunamaanisha umepewa neema ya kuendelea.

Karibu tusikilize, tutafakari na kujifunza pamoja. 🙏📖✨

Listen Now

Love PodBriefly?

If you like Podbriefly.com, please consider donating to support the ongoing development.

Support Us